Matthew 16

Mafarisayo Wadai Ishara

(Marko 8:11-13; Luka 12:54-56)

1 aMafarisayo na Masadukayo wakamjia Isa na kumjaribu kwa kumwomba awaonyeshe ishara kutoka mbinguni.

2 bIsa akawajibu, “Ifikapo jioni, mnasema, ‘Hali ya hewa itakuwa nzuri, kwa kuwa anga ni nyekundu.’ 3 cNanyi wakati wa asubuhi mnasema, ‘Leo kutakuwa na dhoruba, kwa sababu anga ni nyekundu na mawingu yametanda.’ Mnajua jinsi ya kupambanua kule kuonekana kwa anga, lakini hamwezi kupambanua dalili za nyakati. 4 dKizazi kiovu na cha uzinzi kinatafuta ishara, lakini hakitapewa ishara yoyote isipokuwa ishara ya Yona.” Isa akawaacha, akaenda zake.

Chachu Ya Mafarisayo Na Masadukayo

(Marko 8:14-21)

5 eWanafunzi wake walipofika ng’ambo ya bahari, walikuwa wamesahau kuchukua mikate. 6 fIsa akawaambia, “Jihadharini. Jilindeni na chachu ya Mafarisayo na ya Masadukayo.”

7Wakajadiliana wao kwa wao, wakisema, “Ni kwa sababu hatukuleta mikate.”

8 gIsa, akifahamu majadiliano yao, akauliza, “Enyi wa imani haba! Mbona mnajadiliana miongoni mwenu kuhusu kutokuwa na mikate? 9 hJe, bado hamwelewi? Je, hamkumbuki ile mikate mitano iliyolisha watu 5,000 na idadi ya vikapu vingapi vya mabaki mlivyokusanya? 10 iAu ile mikate saba iliyolisha watu 4,000 na idadi ya vikapu vingapi vya mabaki mlivyokusanya? 11Inakuwaje mnashindwa kuelewa kwamba nilikuwa sisemi nanyi habari za mikate? Jilindeni na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo.” 12 jNdipo wakaelewa kwamba alikuwa hasemi juu ya chachu ya kutengeneza mikate, bali juu ya mafundisho ya Mafarisayo na Masadukayo.

Petro Amkiri Isa Kuwa Ni Mwana Wa Mungu

(Marko 8:27-30; Luka 9:18-21)

13 kBasi Isa alipofika katika eneo la Kaisaria-Filipi, akawauliza wanafunzi wake, “Watu husema kwamba mimi Mwana wa Adamu ni nani?”

14 lWakamjibu, “Baadhi husema ni Yahya Mbatizaji; wengine husema ni Ilya; na bado wengine husema ni Yeremia au mmojawapo wa manabii.”

15Akawauliza, “Je, ninyi mnasema mimi ni nani?”

16 mSimoni Petro akamjibu, “Wewe ndiwe Al-Masihi,
Al-Masihi maana yake ni Masiya , yaani Aliyetiwa mafuta.
Mwana wa Mungu aliye hai.”

17 oNaye Isa akamwambia, “Heri wewe, Simoni Bar-Yona,
Bar-Yona ni neno la Kiaramu, maana yake ni Mwana wa Yona.
kwa maana hili halikufunuliwa kwako na mwanadamu, bali na Baba yangu aliye mbinguni.
18 qNami nakuambia, wewe ndiwe Petro na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu, hata malango ya Kuzimu hayataweza kulishinda. 19 rNitakupa funguo za Ufalme wa mbinguni, na lolote utakalolifunga duniani litakuwa limefungwa Mbinguni, nalo lolote utakalofungua duniani litakuwa limefunguliwa mbinguni.” 20 sKisha akawakataza wanafunzi wake wasimwambie mtu yeyote kwamba yeye ndiye Al-Masihi.

Isa Anatabiri Juu Ya Kifo Chake

(Marko 8:31–9:1; Luka 9:22-27)

21 tTangu wakati huo, Isa alianza kuwaeleza wanafunzi wake kwamba hana budi kwenda Yerusalemu na kupata mateso mengi mikononi mwa wazee, viongozi wa makuhani, na walimu wa sheria, na kwamba itampasa auawe lakini siku ya tatu kufufuliwa.

22Petro akamchukua kando, akaanza kumkemea akisema, “Haiwezekani, Bwana! Jambo hili kamwe halitakupata!”

23 uLakini Isa akageuka na kumwambia Petro, “Rudi nyuma yangu, Shetani! Wewe ni kikwazo kwangu. Moyo wako hauwazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu.”

24 vNdipo Isa akawaambia wanafunzi wake, “Mtu yeyote akitaka kunifuata, ni lazima ajikane mwenyewe, auchukue msalaba wake, anifuate. 25 wKwa maana yeyote anayetaka kuyaokoa maisha yake atayapoteza, lakini yeyote atakayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu atayapata. 26 xKwa maana, je, itamfaidi nini mtu kuupata ulimwengu wote, lakini akayapoteza maisha yake? Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake? 27 yKwa maana Mwana wa Adamu atakuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika zake, naye ndipo atakapomlipa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake. 28 zNawaambia kweli, baadhi yenu hapa hawataonja mauti kabla ya kumwona Mwana wa Adamu akija katika Ufalme wake.”
Copyright information for SwhKC